Last Updated on 06/09/2022 by Tabibu Fadhili Paulo
Dodoma. Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, imeshtushwa na kasi ya kuvunjika kwa ndoa nchini chanzo kikubwa kikiwa ni kumomonyoka kwa maadili huku Mkoa wa Dar es Salaam pekee ndoa ni zaidi ya 300 zikivunjika kwa mwezi.
Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Stanslaus Nyongo, leo Jumatatu Septemba 5, 2022 baada ya kukutana na wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia na makundi Maalum.
“Tumepata hesabu (ya ndoa kuvunjika) kwa mfano Dar es Salaam pekee yake zaidi ya ndoa 300 kwa mwezi zinavunjika. Hili tunaona ni tatizo kubwa ni janga. Sisi kama kamati tunaona haja kubwa ya kuishauri Serikali kuona jinsi gani kuchukua hatua kwa ajili ya kupambana na hali hii iliyopo,”amesema.
“Hili limeshamiri sana katika jamii yetu. Na kwakweli kuna haja ya Serikali kutafuta kwa kina chanzo nini na kuona ni hatua gani za kuchukua,” amesema.
Amesema watu wanaona ndoa kama ni jambo tu la kupita na kwamba watu wanaoana baada ya muda mfupi wanaachana.
Aidha, Nyongo amesema kuna ushauri ambao wameutoa kwa Serikali na utatolewa bungeni kuhusu mauaji yanayotokea baina ya wanandoa.
“Tumeona mmonyoko mkubwa wa maadili na ukatili mkubwa wa kijinsia hasa wa watoto ni mkubwa inahitaji Watanzania wajipange,”amesema.
Amesema ukatili umeongezeka unaoweza kusababishwa na vyanzo vingi ikiwemo ugumu wa maisha unaweza na kwamba Serikali ina jambo kubwa la kufanya kuondokana na hilo.
Amesema hilo ni tatizo kubwa na ni janga ambapo kamati imeona kuna haja ya kuishauri Serikali kuona jinsi ya kuchukua hatua maalum ya kupambana na hali iliyopo.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuliona hili na kuamua kuanzisha Wizara hii maalum, aliona kuna tatizo kubwa la ukatili, watu kuathirika kiakili na haya yote yapo kwenye jamii yetu,” amesema.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa wizara, Waziri wa wizara hiyo, Dk Dorothy Gwajima amesema katika kukabiliana na tatizo hilo vitendo vya ukatili katika jamii wizara yake imeendelea kuelimisha jamii ambapo baadhi ya wananchi wameelewa na kuhamasika kuhusu ukatili wa kijinsia na watoto.
Amesema wizara imeunga mkono Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) kwenye mikoa yote 26 ya Tanzania