Last Updated on 23/01/2022 by Tabibu Fadhili Paulo
Sababu zingine 6 za mke kupoteza hamu ya kutaka kushiriki tendo la ndoa
Kesi za wanawake kupoteza hamu ya tendo la ndoa zimezidi kuongezeka tangu mwanzoni mwa mapinduzi ya viwanda hapo mwanzoni mwa karne ya 19.
Kila mtu ana sababu zake juu ya kuongezeka kwa tatizo hili.
Mwanamke kukosa au kuishiwa hamu ya tendo la ndoa ni moja kati ya sababu zinazoweza kupelekea kuvunjika kwa mahusiano baina ya mme na mke
Wanaume wengi wazo la kwanza linalowajia kichwani wakati wake zao wanapokuwa na tatizo la kupungukiwa hamu ya tendo la ndoa ni kuwa mwanamke huyo ameanza uhuni na ana michepuko.
Siyo lazima mkeo awe na michepuko ndiyo apungukiwe na hamu na wewe.
Kuna mwanamke anaweza kuwa na michepuko na bado asiishiwe na hamu na mme wake.
Basi leo nimeakuandikia sababu 6 zingine zaidi zinazoweza kupelekea mkeo kuishiwa hamu ya tendo la ndoa.
Huko nyuma nimewahi kuandika sababu zingine 10 tofauti na hizi za leo na nitakupa link pale mwishoni mwa makala hii.
Sababu zingine 6 za mke kupoteza hamu ya tendo la ndoa ;
1. Yupo bize sana na kazi
Kama mkeo naye ameajiriwa sehemu anafanya kazi au ana biashara yake binafsi na muda mwingi ametingwa na shughuli hizo na wakati huo huo majukumu ya nyumbani ya kupika, kufua, kuangalia watoto yote yanamsubiri yeye ni rahisi sana kupungukiwa na hamu ya kutaka kushiriki tendo la ndoa.
Suluhisho la tatizo : Mme ajaribu kumsaidia mkewe baadhi ya kazi za nyumbani ili kumpatia mkewe muda wa kupumzika baada ya kutoka kazini.
Ikiwezekana mnaweza kuajiri Dada wa Kazi ili kumpunguzia mke majukumu.
Kama baba nawe unafanya kazi na hela unapata na hamna mahitaji mengi labda tayari mmejenga nyumba yenu hivyo hamdaiwi kodi ya nyumba unaweza kumwambia mkeo apumzike nyumbani aangalie familia.
Siyo lazima mke awe mtafutaji na mhangaikaji, mnaweza kukubaliana mkeo apumzike nyumbani na wewe mme uendelee na kazi na kukimbizana huko kwenye madaladala.
2. Hamu yake ipo chini kidogo tofauti na yako
Binadamu tumetofautiana na hatuwezi kuwa sawa.
Inawezekana mkeo hamu yake ya kutaka kushiriki tendo la ndoa siyo kubwa au haimtokei mara nyingi kama wewe.
Ni tatizo la kawaida na linatokea kwenye ndoa nyingi na kwa watu wa jinsia zote.
Inawezekana mmoja wenu anataka mara 3 kwa wiki na mwingine anataka mara 1 kwa wiki.
Ni jambo la kawaida na linajulikana kwa kitaalamu kama ‘low sex libido’ na tafiti zinasema ndoa moja katika kila ndoa 5 ina tatizo kama hili.
Hapa siyo kwamba mke hakupendi na siyo kwamba ana michepuko, hapana, ila tu hamu yake kwa asili ipo chini.
Suluhisho la tatizo : Mme uongee na mkeo kwa lugha ya upole na bila kuwa na dalili ya kutaka kuhukumu.
Mweleze kiundani namna jambo hilo linavyokukera na nini ungependa kibadilike ili wote kwa pamoja muwe na furaha na kuridhika na ndoa yenu.
Hata hivyo jambo hili ni bora zaidi likizungumzwa mkiwa watu watatu yaani mme, mke na mtaalamu wa masuala ya mapenzi na mahusiano.
Mkiwa wawili tu mnaweza msifikie muafaka mzuri wa tatizo hili.
Kama mpo Dar Es Salaam na maeneo karibu na Dar Es Salaam mnaweza kuja tuonane na mimi nitawasaidia kwa gharama ya shilingi 35000, Weka miadi (appointment) kupitia WhatsApp +255714800175
3. Hapendezwi na aina ya mapenzi unayompa
Hapa ndiyo penye shida kuliko sehemu nyingine yoyote.
Mwanamke anaweza kupoteza hisia za kutaka kushiriki tendo la ndoa hata ndani ya ndoa yenye amani na furaha zote ikitokea aina ya tendo la ndoa analopewa siyo lile analolipenda zaidi.
Inawezekana mme umeng’ang’ania kutaka mshiriki tendo la ndoa kila siku mkiwa kitandani tu kumbe mwenzio anapenda zaidi mshiriki mkiwa jikoni au sebuleni.
Inawezekana mme una tabia ukifika tu kitandani tayari unataka kumlenga mtoto wa watu kumbe mwenzio anapenda umshikeshike kwanza, umtanie, umchezee, umpe glasi moja kwanza ya maji ndiyo muendelee.
Wanawake wengi wanapenda vitu vipya na vya kusisimua kila mara.
Mme uwe na uwezo wa kufahamu staili nyingine nyingi zaidi za kushiriki tendo la ndoa siyo hiyo hiyo moja kila siku mke hakawii kukinai na hatimaye kupungukiwa na hamu ya kutaka kushiriki tendo la ndoa.
Siyo wanawake wote wanaweza kufika kileleni kwa kuwekewa uume ukeni kila siku, wengine wanahitaji zaidi ya hapo.
Wanawake wanapenda mwanaume mtundu na mkorofi kitandani siyo mpole mpole na anawaza kusali wakati mpo kwenye mahaba.
Kila jambo na wakati wake, muda wa kusali salini kweli kweli na muda wa mahaba mfanye mahaba kweli siyo maigizo.
Suluhisho la tatizo : Mme ongea na mkeo kuhusu aina ya mapenzi anayotaka na uwe tayari kumtimizia kama atakavyokujibu.
Kama unataka raha kweli kweli usiwe muoga wa kuongea na mkeo na Kumuuliza yeye anapendezwa na nini na nini hasa muwapo kitandani.
Jambo la mhimu hapa ni kuwa chochote atakachokujibu anakipenda uwe tayari kumpa hata kama mtizamo wako na namna ulivyolelewa vinasema tofauti.
Kwa mfano anaweza kukujibu mara moja kwa mwezi anataka mkalale guest house mrudi nyumbani asubuhi, na wakati huo huo wewe ni mlokole na uliambiwa na kuaminishwa kwamba kulala guest house ni dhambi, basi kazi unayo.
Muulize tu taratibu na kwa upole; ‘mke wangu tukiwa kitandani unapenda niwe nakufanyia nini na nini ili ufurahie zaidi?’
Na uwe tayari kwa jibu lolote atakalokupa.
Ongeza ufahamu na uelewa wako zaidi kuhusu tendo la ndoa.
4. Hakuna muunganiko wa hisia baina yenu wawili
Mapenzi huwa matamu pale mme na mke wanapoishi kama mtu na rafiki yake.
Lazima mzoeane na muwe karibu na kila mmoja asione tabu kueleza ukweli au hisia zake kwa mwenzake.
Je mkeo yupo huru na wewe kwa kiasi gani? Anaweza kukutania kidogo? Anaweza kuvaa kaptula au suruali yako na ukaona poa tu? Anaweza kujamba kwa sauti mbele yako na ukaona poa?
Mara ngapi kwa siku unamwambia unampenda? Ukiwa kazini au kwenye mihangaiko yako huwa unakumbuka kumtumia japo sms tu ya kumkumbuka?
Huwa unamshirikisha kwenye mambo yako na kwenye mambo mengine ya mhimu kuhusu mstakabali wa ndoa yenu na watoto wenu?.
Mke hawezi kuwa na hisia na wewe kama hakuna muunganiko mzuri wa hisia baina yenu wawili.
Kama hakuna ukaribu kati yenu ni rahisi mke kupoteza hisia.
Kuna ndoa watu wanaishi kama mwanafunzi na mwalimu au kama mchungaji na muumini. Hakuna ukaribu wowote, mmoja ni wa kutoa amri na mwingine ni wa kutekeleza amri!
Mapenzi hayapo hivyo.
Lazima kuwe na emotional connection and mutual understanding.
Suluhisho la tatizo : Kuwa karibu na mkeo, taniana naye, nenda naye kutembea huko na huko, mwache awe huru na wewe.
Wasiliana naye mara kwa mara uwapo kazini na kwenye mihangaiko yako mingine.
5. Huenda ana tatizo fulani la kiafya
Matatizo mbalimbali ya kiafya yanaweza kumfanya mwanamke apoteze hamu ya tendo la ndoa.
Mfano kama anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari, maumivu mbalimbali yasiyoisha, saratani, mabadiliko ya homoni, msongo wa mawazo (stress) nk mambo haya yanaweza kumfanya mkeo apoteze hamu ya tendo la ndoa na wewe.
Matatizo mengine kama ya maumivu ukeni wakati wa tendo la ndoa, miwasho na maambukizi ukeni pia vinaweza kumfanya apoteze hamu ya tendo la ndoa.
Suluhisho la tatizo : Kama hujuwi ikiwa anaumwa mojawapo ya matatizo hapo juu mshauri umpeleke hospitali kwa vipimo na uchunguzi zaidi kujua nini kinaendelea kwenye afya yake kwa ujumla.
6. Hapendezwi tena na wewe au na uhusiano wenu
Hapa nikupe pole kabla sijaeleza namna tatizo lilivyo.
Inawezekana mkeo amefikia hatua ambayo hakupendi tena, hakuhitaji na haoni sababu ya kuwa kwenye huo uhusiano wenu.
Mke akifikia hatua hii ni vigumu awe na hamu ya kutaka kushiriki tendo la ndoa na wewe.
Sababu za kufika hatua hii zinaweza kuwa nyingi na nyingine zinaweza kuwa ni za muda mrefu na hazikutafutiwa ufumbuzi wake.
Hata hivyo usifikie hitimisho kwa haraka, huenda ni jambo lingine tu na siyo kwamba hakupendi tena na hataki kuwa na wewe.
Lakini hata kama hakupendi na hahitaji kuwa na wewe siyo jambo baya na wala usijipe huzuni bila sababu, ni jambo la kawaida kubaliana nalo na usilazimishe chochote.
Suluhisho la tatizo : Kuwa na majadiliano ya wazi baina yako na mkeo, muulize ikiwa hakupendi tena au hapendi tena mahusiano yenu na uwe tayari kupokea lolote atakalokujibu.
Usilazimishe mapenzi, kama mwenzio haoni sababu ya kuwa na wewe basi isiwe tabu na isiwe vita.
Mnaweza kuachana kwa amani bila fujo wala matangazo na mhimu kuliko yote ruhusu maisha mengine yaendelee.
Kumbuka kutunza amani, maisha ni mhimu zaidi kuliko mali za kidunia au mahusiano ya hapa duniani, vyote tutaviacha siku moja.
Soma sababu zingine 10 za mke kupoteza hamu ya tendo la ndoa kwa kubonyeza hapa